Mahakama moja ya Misri jana Jumamosi ilimhukumu mtu mmoja adhabu ya kifo kwa kuuwa kwa kumchoma kisu Kasisi wa Kanisa la madhehebu ya Koptiki mwezi Aprili katika shambulio lililoshtua taifa hilo lenye watu wengi zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu.
Nehru Tawfiq, mwenye umri wa miaka 60, alipatikana na hatia katika mahakama ya jinai ya Alexandria kwa mauaji ya Kasisi Arsanious Wadid mwenye umri wa miaka 56 na kupatikana na kisu kinyume cha sheria. Mawakili wake walikuwa wamedai kuwa mauaji hayo hayakuwa ya makusudi. Tawfiq anaweza kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Wadid aliuawa katika eneo maarufu la bahari katika mji wa Alexandria mwezi Aprili.