Korea Kaskazini yafanya gwaride la kijeshi bila makombora ya masafa marefu

Vifaru vya kijeshi vikipita wakati wa maandamano ya kuadhimisha miaka 70 tangu taifa hilo kuundwa huko Pyongyang, North Korea, Jumapili, Septemba 9, 2018.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Jumapili amekuwa mgeni rasmi kwenye gwaride kubwa la kijeshi, kusheherekea miaka 70 tangia taifa hilo kuundwa, lakini mwaka huu jeshi halikuonyesha makombora yake yaliyoboreshwa ya masafa marefu.

Hata hivyo Kim Jong Un hakutoa hotuba yoyote kwa umati uliyohudhuria katika uwanja wa Pyongyang Kim II.

Gwaride hilo lilionyesha vifaru vya kijeshi, makombora ya kawaida na vikosi vingine kutoka katika matawi yote ya jeshi la nchi hiyo.

Badala yake, msititizo uliowekwa mwaka huu ni hatua za kiraia zinazochukuliwa zikilenga kujenga uchumi wa Korea.

Gwaride hili la kijeshi limefanyika katika wakati huu nyeti kwa hali ilivyo nchini Korea Kaskazini.

Nchi hii inajaribu kupunguza mvutano ulioko baina yake na Marekani, kufuatia mkutano wa ngazi ya juu kati ya Kim na Rais wa Marekani Donald Trump mapema mwaka 2018 huko Singapore.

Viongozi wote wawili wanataka makubaliano yafikiwe kabla ya mazungumzo mapya kuanza. Washington inataka Korea Kaskazini itoe ahadi ya kuangamiza silaha zake za nyuklia, wakati Pyongyang inataka ihakikishwe usalama wake na kupewa nafuu nyingine mapema kabla ya kufanya hivyo.