Kontena lenye pembe za ndovu lakamatwa Zanzibar

Baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa na meno ya tembo

Vikosi vya ulinzi na usalama zanzibar kwa kushirikiana na raia wema wamefanikiwa kukamata kontena la futi 40 likiwa na pembe za ndovu zilizohifadhiwa katika mabaki ya mazao ya baharini likiwa katika mpango wa kusafirishwa nje ya nchi kupitia bandari ya Malindi visiwani Zanzibar.

Your browser doesn’t support HTML5

Ripoti ya Munir Zacharia, Zanzibar


Kontena hilo limekamatwa majira ya alasiri na askari wa jeshi la polisi kikosi cha kuzuia magendo-KMKM, usalama wa taifa ambao mara moja walianza kazi ya kupasua kila gunia na kufanikiwa kupata pembe za ndovu zikiwa zimehifadhiwa katikati ya mazao ya baharini maarufu kwa jina la Shell.

Akizungumza na waandishi wa habari, waziri wa maliasili na utalii, Khamis Kagasheki amesema wakati umefika kwa Watanzania kupiga vita vitendo vya ujangili vinavyofanywa na watu wachache kwa manufaa yao binafsi bila ya kutafakari kuwa vitendo hivyo vitawamaliza wanyama ambao ni maliasili ya taifa.

Wakati huo huo waziri wa nchi ofisi ya rais tawala za mikoa na idara maalum, Haji Omar Kheir amesema watu waliohusika na tukio hilo watafikishwa katika vyombo vya sheria baada ya kukamilika kwa taratibu za uchunguzi na kushtakiwa kwa sheria ya uhujumu uchumi.

Hii ni mara ya pili kukamatwa kwa nyara za serikali katika kipindi cha miaka miwili katika bandari ya Malindi mjini Zanzibar ambapo kontena la futi 20 lilikamatwa likiwa katika mpango wa kusafirishwa kuelekea nchini China.