Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa tathmini kuhusu hali ya Korea Kaskazini, Jumatano, muongo mmoja baada ya ripoti ya kina kueleza hali halisi ya unyanyasaji mkubwa na ulioenea nchini humo.
“Leo hii, Korea Kaskazini ni nchi iliyotengwa na ulimwengu,” Volker Turk, ameuambia mkutano maalum wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambao balozi wa Korea Kaskazini hakuhudhuria.
Amesema kuna hali ya kushangaza na kuchukiwa ndani ya DPRK ambapo maisha ya kila siku ya watu ni magumu na hakuna matumaini. DPRK ni kifupi cha jina rasmi la Korea Kaskazini, yaani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea.
Turk ameonyesha wasiwasi wake kuhusu udhibiti mkali wa serikali wa mienendo ya raia wake pamoja na uwezo wao wa kuondoka nchini humo.