Jill Biden kuongoza timu ya Marekani kwenye Olimpiki, Japan

Mke wa rais wa Marekani Jill Biden kwenye picha ya awali.

Mke wa rais wa Marekani Jill Biden Jumatano amefanya ziara yake ya kwanza ya kimataifa akiwa peke yake, wakati akiongoza ujumbe wa Marekani kwenye michezo ya Olimpiki mjini Tokyo Japan.

Jill aliondoka Washington na kisha kutua Alaska kwanza ili kuzungumza na wanajeshi pamoja na kuhimiza umuhimu wa kupata chanjo ya covid.

Kiongozi huyo anatarajiwa kuwasili Tokyo Alhamisi na kisha kukutana na waziri mkuu wa Japan Yoshihide Suga, kabla ya kuhudhuria ufunguzi wa michezo hiyo Ijumaa, na kisha kuondoka Jumamosi akipitia Hawaii kuitembelea kliniki moja ya chanjo huko kabla ya kurejea mjini Washington.

Msemaji wa ikulu ya Marekani Jen Psaki alisema kuwa Rais Joe Biden na mke wake Jill Biden, waliona ni muhimu kwa timu ya Marekani kusindikizwa na mtu wa ngazi ya juu, ili kuwapa motisha wakati huu mgumu kutokana na janga la corona.

Atakapokuwa nchini Japan Jill Biden pia atakuwa na mkutano kwa njia ya mtandao na timu ya Marekani pamoja na kutembelea Emperor wa Japan Naruhito kwenye makao yake ya kifalme.