Idadi ya vifo kutokana na mafuriko nchini Afghanistan yafikia 300

  • VOA News

Miili ya watu waliofariki katika mafuriko makubwa katika jimbo la Baghlan kaskazini mwa Afghanistan, Mei 11, 2024. Picha ya AP

Umoja wa Mataifa na mamlaka za Taliban Jumamosi wamesema idadi ya vifo kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa za msimu zilizonyesha katika jimbo la kaskazini mwa Afghanistan la Baghlan imeongezeka na kufikia watu 300.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema mafuriko hayo yaliharibu zaidi ya nyumba 1,000. Limesema kwamba “haya ni moja ya mafuriko mengi yaliyotokea katika wiki chache zilizopita kutokana na mvua kubwa zisizo za kawaida.

Afisa mkuu wa utawala wa Taliban amesema katika ujumbe wa video kwenye mtandao wa kijamii kwamba janga la Ijumaa lilisababisha vifo vya watu 150 katika wilaya pekee huko Baghlan inayoitwa Nahreen.

Ghulan Rasool Qani amesema idadi ya vifo inaweza kuongezeka na kubaini kuwa helikopta za kijeshi ziliwasili katika eneo hilo kuwasaidia katika shughuli za uokoaji.

Msemaji wa serikali ya Taliban Zabihullah Mujahid alisema kwenye mtandao wa X kwamba mafuriko yalisababisha uharibifu katika majimbo mengine kadhaa ya kaskazini na magharibi mwa nchi, yakiwemo Badakhshan, Ghor na Herat.