Hospitali ya mwisho inayofanya kazi katika El-Fasher magharibi mwa Sudan imefungwa baada ya shambulio la wanamgambo wanaojaribu kuuteka mji muhimu wa Darfur, limesema shirika la madaktari wasio na mipaka.
Vita vimeendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja kati ya jeshi lililo chini ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na wanamgambo wa Rapid Support Forces wanao-ongozwa na naibu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo.
El-Fasher iliyoko North Darfur ni mji mkuu pekee wa jimbo katika mkoa mkubwa wa magharibi ambao hauko chini ya udhibiti wa RSF, ni kituo muhimu cha kibinadamu kwa eneo hilo lililo kwenye ukingo wa kukumbwa na njaa.
“Jumamosi, MSF na wizara ya afya walisitisha shughuli zote katika South Hospital, El-Fasher, North Darfur, baada ya wanamgambo wa RSF kushambulia kituo hicho, kufyatua risasi na kupora mali, ikiwa ni pamoja na kuiba gari la wagonjwa la MSF,” ilisema NGO hiyo katika taarifa iliyotumwa Jumapili jioni kwenye mtandao wa X.