Mawaziri wa Nigeria wapinga Rais kujiuzulu

Baraza la mawaziri la Nigeria limekataa wito wa kujiuzulu Rais Umaru Yar’Adua, ambaye amekuwa hospitali kwa siku 9 zilizopita huko Saudi Arabia.

Baraza la mawaziri lilitoa taarifa jana Jumatano likisema mawaziri kwa kauli moja waliamua hakuna msingi wa kutumia kipengele cha katiba kinachowaruhusu kumuondoa Rais madarakani.

Katiba ya Nigeria inasema Rais anaacha madaraka kama baraza la mawaziri, kwa wingi wa theluthi mbili linapitisha azimio la kutangaza hawezi kufanya kazi yake. Tangazo hilo lazima lithibitishwe na wataalamu wa afya ambao ni pamoja na daktari binafsi wa Rais.