Kiongozi wa Mungiki aachiwa huru

Kiongozi wa kundi lililopigwa marufuku nchini Kenya la Mungiki, Maina Njenga, ameachiwa huru Ijumaa baada ya kuwa kizuizini kwa muda mrefu kutokana na shutuma za kukabiliwa na makosa ya mauaji.

Serikali ya Kenya kupitia mwanasheria mkuu ilisimamisha kesi dhidi ya kiongozi huyo ambaye amekuwa akipambana kortini kufuatia mashtaka ya mauaji yaliyokuwa yakimkabili.

Kiongozi huyo wa kundi la Mungiki alikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya watu 29 ambapo maafisa wa polisi walidai mauaji hayo yalifanywa na wafuasi wa kundi lake kufuatia agizo la kiongozi huyo. Mara baada ya kuachiwa huru kiongozi huyo alisema ana furaha na sasa anataka mwanzo mpya wa maisha bora.

Viongozi wa kitengo cha kisiasa cha Mungiki-Kenya National Youth Alliance, wakiongozwa na Njuguna Gitau wameunga mkono kuachiliwa huru kwa kiongozi huyo.