Zaidi ya 30 Wauawa Kenya

Polisi nchini Kenya wanasema watu wasiopungua 29 wamekufa baada ya mapigano kati ya wakazi wa eneo moja nchini humo na wafuasi wa genge la uharifu lililopigwa marufuku. Machafuko hayo yalianza Jumatatu jioni, baada ya wanavijiji nje na ndani ya mji wa Katarina kujiandaa kwa mapigano na genge la Mungiki.

Wanavijiji wanasema kundi hilo katili ambalo liko kama mafia limekuwa likiendesha shughuli zake hivi karibuni katika eneo hilo. Mashahidi wanasema makundi ya watu yalishambulia usiku makazi ya watu wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa Mungiki, wakiwaburuza mitaani na kuwaua kwa kutumia mapanga, shoka na biboko. Watu wasiopungua 40 wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na machafuko hayo.

Mwandishi wa Sauti ya Amerika anaripoti kuwa mauaji hayo yamefanyika baada ya ushirikiano kati ya polisi na wanajamii kupambana na kundi la Mungiki na kuzidisha oparesheni za kuwasaka na hatimaye kuwaua wafuasi hao wa Mungiki.