Serikali ya Tanzania Yashitakiwa

Kituo cha sheria na haki za binadamu, kikishirikiana na chama cha maalbino nchini Tanzania, kimeishitaki serikali ya nchi hiyo kupitia mwanasheria mkuu kwa kushindwa kuwalinda walemavu wa ngozi wanaojulikana kama albino dhidi ya mauaji.

Akiongea na Sauti ya Amerika Ijumaa kwa njia ya simu, mtetezi wa haki za binadamu, Clarence Kipobota alisema kuwa wameamua kuifungulia mashitakai serikali ya Tanzania kwa madai kuwa imekiuka katiba ya nchi.

Bwana Kipobota alisema kuwa serikali ya Tanzania imeshindwa kuwapatia watu wenye ulemavu wa ngozi haki ya kulindwa dhidi ya athari zinazotokana na jua kali, ambalo linaweza kuwasababishia matatizo kadhaa ya mwili, ikiwemo kansa ya ngozi.

Muhimu zaidi, anasema Bwana Kipobota, serikali imevunja kipengele cha katiba kinachosema kila mtu anahaki ya kuishi, kwa kushindwa kuwalinda maalbino ambao wamekuwa wakiuawa kwa imani za kishirikina katika miezi ya hivi karibuni.