Kenyatta atoa wito wa tahadhari barabarani kipindi cha mwisho wa mwaka

Basi lililogongwa kwenye ajali ya magari katika barabara kuu Eldoret na Nakuru

Akiongoza maadhimisho ya miaka 54 ya Kenya kujitangazia uhuru, Rais Uhuru Kenyatta amewataka madereva kuwa waangalifu msimu huu wa Krismasi.

"Sasa wakati tunaelekea katika siku kuu ya Kritsmasi na Mwaka Mpya ninataka niwaombe wa-Kenya, hasa madereva wetu, tafadhalini tujichunge kwenye barabara zetu. Hii siku chache tumepoteza waimbaji wetu, na mahala hapo hapo palitokea ajali juzi na leo hii huko Bungo9ma ajali imesababisha vifo vya wa-Kenya wengine. Basi tujichunge wakati huu."

Wito huo ametoa Jumanne, siku moja tu baada ya ajali mbaya ya barabara kufanyika na kuwaua watu takribani 14 katika barabara kuu ya Kitale -Webuye magharibi ya Kenya.

Your browser doesn’t support HTML5

Wandera aripoti ajali mbaya kwenye barabara kuu kati ya Nakuru-Eldoret

Ajali nyingine imetokea siku ya Uhuru Jumanne Disemba 12 katika barabara kuu ya Eldoret-Nakuru na kuwaua watu 13 huku wengine wengi wakijeruhiwa na kupelekwa katika hospitali kadhaa katika kaunti ya Nakuru.

Kwa mujibu wa afisa mkuu wa Trafiki ukanda wa Bonde la Ufa, Ziro Arome, watu kumi na watatu wamepoteza maisha yao papo hapo na wengine wengi kujeruhiwa vibaya katika eneo la Sachangwan wakati magari yasiyopungua kumi na matatu kuhusika katika ajali ya barabara mapema Jumanne asubuhi.

Ajali hii inajiri tu saa chache baada ya ajali nyingine kufanyika karibu na daraja la Kamkuywa kwenye barabara ya Kitale-Webuye na kuwaua watu kumi na wanne na wengine wengi kupata majeraha makubwa na kulazwa katika hospitali ya Kimilili.