Kenya yatangaza ukame kuwa janga la kitaifa

Rais Uhuru Kenyatta akihutubia sherehe za Jamhuri Day za mwaka 2016. Februari 10, 2017, Kenyatta alitangaza hali ya kiangazi nchini Kenya kuwa janga la kitaifa.

Serikali ya Kenya, imesema kuwa hali ya ukame inayoendelea nchini ni janga la kitaifa.

Akizungumza katika ikulu ya Nairobi Ijumaa baada ya kukutana na baraza lake la mawaziri, Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa ni kaunti 23 ndio zilizoathiriwa mno na hali ya ukame.

Aidha Kenyatta aliwataka wadau wote kuimarisha programu ambazo zitakabiliana na hali hiyo tete.

Amesema kuwa ukame tayari umekwisha waathiri binadamu, mimea na mifugo, akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, kusaidia juhudi za serikali yake katika kukabiliana na tatizo hilo.

Taarifa iliyotolewa na ikulu ya Nairobi imesema kuwa wizara ya fedha imetoa shilingi milioni 7.3, huku serikali za kaunti zikitoa shilingi milioni 2, katika juhudi za kukabiliana na hali hiyo.

Idara ya hali ya hewa nchini Kenya imekuwa ikionya kuwa ukame utaendelea hadi kuanza kwa mvua zinazotarajiwa mwezi Aprili.