Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 15:16
VOA Direct Packages

WHO laomba msaada wa kimataifa, ili kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu, Africa


Dkt Matshidiso Moeti, mkuu wa WHO tawi la Afrika.
Dkt Matshidiso Moeti, mkuu wa WHO tawi la Afrika.

Afisa mmoja wa shirika la Afya Duniani WHO, barani Afrika ameomba misaada zaidi kwa mataifa yanayokabiliwa na mlipuko wa kipindupindu, akisema  kuwa ugonjwa huo huenda ukasambaa zaidi  kutokana na mvua zinazoendelea kwenye baadhi ya maeneo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, Dkt Patrick Otim ambaye ni afisa wa dharura wa WHO amesema kwamba milipuko ya kipindupindu ni hatari kutokana na maambukizi ya haraka pamoja na maeneo yenye maji yaliyosimama.

Amesema ni muhimu kutoa misaada kwa mataifa hayo ili yakabiliane na milipuko kabla haijaenea zaidi. Kufikia sasa kipindupindu kimeripotiwa kwenye mataifa 12 kati ya 54 yaliyopo Afrika. Kesi za karibu zaidi zimeripotiwa Afrika Kusini, Tanzania na Zimbabwe. Malawi imeshuhudia mamia ya vifo kutokana na mlipuko unaosemekana kuwa mbaya zaidi nchini humo.

Kisiwa cha Madagascar ambacho kimekumbwa na vimbunga viwili mwaka huu pia kinakabiliwa na mlipuko wa kipindupindu. Kipindupindu ni ugonjwa unaoenezwa na maji machafu, na mkuu wa WHO barani Afrka Dkt Matshidiso Moeti amesema kwamba ongezeko la mvua kwenye mataifa kama Malawi linapunguza juhudi za kudhibiti mlipuko uliopo.

WHO limeonya kuwa mabadiliko ya hali ya hewa huenda yakaongeza milipuko ya kipindupindu, kwa kuwa bakteria wanaosababisha ugonjwa huo huzaana kwa kasi zaidi, kwenye maeneo yenye maji yenye joto. Kufikia sasa, chanjo za kumeza kwa mdomo milioni 3.4 zimetumwa Kenya, Congo na Msumbiji, ambako kesi za maambukizi zinaendelea kuongezeka.

XS
SM
MD
LG