Maafisa wa zima moto wanasema miili tisa imepatikana kutoka kwenye vifusi vya moto mkubwa katika jengo linalotumika wakati wa likizo huko mashariki mwa Ufaransa ambapo watu 11 waliripotiwa kupotea.
Moto huo ulizuka Jumatano asubuhi katika mji wa Wintzenheim. Maafisa wanasema nyumba hiyo ilikodishwa na chama ambacho kinawasaidia watu wenye ulemavu. Wakazi hao ambao hawajulikani waliko wakiwemo watu wazima 10 wenye ulemavu na mfanyakazi mmoja walikuwa wanatokea mji wa mashariki wa Nancy.
Christopher Marot, kiongozi wa wilaya ya Haut-Rhin aliwaambia waandishi wa habari mapema Jumatano kwamba hakuna ishara kwamba watu 11 waliopotea, walifanikiwa kukimbia moto huo. Moto huo ulidhibitiwa haraka, lakini Waziri wa Mambo ya Ndani Gerald Darmanin aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, ambao zamani ulijulikana kama Twitter kwamba vifo kadhaa vimeripotiwa kutoka eneo la tukio na kwamba shughuli za uokoaji bado zinaendelea.
Watu wengine 17 waliokolewa kutoka kwenye moto huo, huku mtu mmoja akisafirishwa hadi hospitali iliyo karibu. Waziri Mkuu wa Ufaransa, Elisabeth Borne amesema kupitia mtandao wa X kwamba anaelekea eneo la tukio hilo. Sala yangu ya kwanza ni kwa waathirika na wapendwa wao, aliandika.
Forum