Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Januari 19, 2025 Local time: 05:12

Wadau waiomba Serikali ya Tanzania kuzidi kupambana na ukatili kwa watoto


Mkuu wa wilaya ya Tanga Tanzania Hashim Mgandilwa akizungumza na wananchi katika semina ya kumlinda mtoto.
Mkuu wa wilaya ya Tanga Tanzania Hashim Mgandilwa akizungumza na wananchi katika semina ya kumlinda mtoto.

Kutokana na kuongezeka  kwa matukio ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto nchini  Tanzania, Viongozi  wa dini na wadau wa maendeleo wameitaka  Serikali kutoa mafunzo endelevu kwa waandishi wa habari.

Rai hiyo ya mafunzo iketolewa ili kuwajengea uelewa wa kutosha kuhusu athari ya matukio hayo huku wanahabari wakitakiwa kuwa umakini sana na suala hili na kutumia fursa waliyonayo kuielimisha jamii.

Kasi ya matukio ya ukatili nchini Tanzania inazidi kuleta mashaka na wasiwasi mkubwa kwa wazazi na walezi huku mmomonyoko wa maadili katika jamii ukishuhudiwa kwa kiwango kikubwa na kuelezea hali hii pia imechangiwa na utandawazi hivyo kutishia usalama wa watoto.

Libe Chonya Mhadhiri kutoka chuo kikuu huria Tanzania anaiomba Serikali kutilia uzito jambo hili katika kupambana nalo kwa kuhakikisha elimu inapewa nafasi kubwa zaidi kwa kila daraja la elimu ili kutokomeza kabisa ukatili huu.

Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto katika taifa hili vimeathiri kwa kiasi kikubwa familia nyingi huku ufumbuzi wake ukionekana bado upo nyuma katika kuwalinda watoto.

Padri Odilo Shedafa kutoka Jimbo katoliki katika Mkoa wa Tanga anaamini Waandishi wa habari ni watu muhimu zaidi watakaosaidia mapambano dhidi ya ukatili huu kwa kuwataka kuwa mstari wa mbele katika kuibua taarifa za matukio hayo pamoja na kutoa elimu kwa Jamii .

Kwa upande wake Mkurugenzi wa asasi ya kiraia Tayota inayosimamia haki za watoto mkoani Tanga George Bwire amesema namna bora ya Serikali kukomesha hali hii ni kubadilisha sheria zake zilizopo sasa ambazo zinaonekana kutoa mwanya zaidi kwa watuhumiwa wa matukio ya ukatili hasa inapotokea uwepo wa udugu kati ya mtuhumiwa na aliyefanyiwa ukatili.

Malalamiko ya walio wengi juu ya matukio hayo ya ukatili yanaleta taswira kuwa jambo hili limeleta matokeo mabaya kwa waathiriwa wa vitendo hivyo. Kama Serikali pamoja na wazazi na walezi hawatakuwa imara katika kuwasimamia watoto wao ndoto za vijana wengi zitaishia njiani.

Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam

XS
SM
MD
LG