Waasi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaonya kuwa wataingia katika mji mkuu Bangui hivi karibuni, licha ya makubaliano kati yao na serikali kuwa watafanya mazungumzo yasio ya masharti mapema Januari. Jumapili mitaa ya mji mkuu haikuwa na watu na wakazi wengi mjini humo walisema wamenunua vyakula na bidhaa za kimsingi na kuvihifadhi wakihofia kuwa waasi huenda wakaingia mjini humo. Tishio la waasi hao limetolewa wiki tatu baada ya kuanza maasi dhidi ya serikali. Katika kipindi hicho wamedhibiti thuluthi moja ya nchi na kuwalazimisha wanajeshi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kurudi nyuma hadi mji wa Damara, mji unaopakana na mji mkuu Bangui yapata kilomita 75 tu. Mkuu wa Umoja wa Afrika kwa sasa Thomas Yayi Boni anatazamiwa kwenda nchini humo kukutana na rais Francois Bozize, katika juhudi za kuanza upya mazungumzo ya amani na Seleka, kundi mseto la waasi wenye silaha nchini humo. Seleka linashtumu rais Bozize kwa kushindwa kutekeleza kikamilifu mkataba wa amani uliofikiwa mwaka wa 2007. Mkataba huo ulijumwisha makubaliano ya kuyashirikisha makundi ya wapiganaji kwenye jeshi la kitaifa na kuwalipa ikiwa watakaosalimisha silaha zao kufuatia maasi ya hapo awali.
Waasi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wasema wataingia mji mkuu Bangui licha ya kukubali kufanya mazungumzo na serikali Januari.