Bunge la Uganda linatafakari nyongeza ya mshahara kwa asilimia 100 kwa maafisa wote wa tume ya uchaguzi nchini humo kabla yan uchaguzi mkuu mwezi Februari.
Maafisa wa tume hiyo hawajapata nyongeza ya mshahara tangu 1999 na baadhi ya wabunge wanasema wakati umefika. Wabunge hao wanasema wafanyakazi wengine wa idara za umma, ikiwa ni pamoja na waalimu, wamepata nyongeza moja au zaidi katika kipindi hicho.
Hatua hiyo imekuja baada ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi badru kiggundu kuhimiza wabunge waidhinishe nyongeza ya mshahara kulingana na gharama za maisha.
Hata hivyo, vyama vya upinzani na jamii za kiraia zinasema kuna uwezekano mdogo serikali ya Rais Yoweri Museveni itatenga fedha kwa ajili ya nyongeza hiyo. Wanadai kuwa utawala wa Museveni uko tayari kutumia fedha kuhakikisha anashinda uchaguzi wa Februari kuliko kulipa wafanyakazi wa tume ya uchaguzi.
Serikali ya Rais Museveni haijatoa tamko lolote kuhusu pendekezo hilo.