Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 18, 2024 Local time: 20:38

Somalia yapanga kuimarisha jeshi la kitaifa


Majeshi ya Umoja wa Afrika (AMISOM) yakiwa Dhobley, Somalia, September 30, 2012.
Majeshi ya Umoja wa Afrika (AMISOM) yakiwa Dhobley, Somalia, September 30, 2012.

Waziri wa ulinzi Abdihakim Haji Mohamud Fiqi asema jeshi thabiti la kitaifa litakalowakilisha kanda zote za nchi ni kipaumbele cha wizara yake.

Waziri wa ulinzi wa Somalia anasema kushirikisha makundi ya wanamgambo wa Koo mbalimbali katika jeshi la kitaifa ni changamoto kubwa kwa jeshi hilo huku ikijitahidi kudhibiti hali ya usalama nchini humo. Akizungumza katika mahojiano na Sauti ya Amerika mjini Mogadishu, waziri wa ulinzi wa Somalia Abdihakim Haji Mohamud Fiqi alisema hatua ya kushirikisha makundi mbali mbali katika jeshi la kitaifa kuwakilisha kanda za nchi ni kipaumbele cha wizara yake.

Alisema wanajeshi wapya wanaandikishwa katika ngazi za kijeshi kote nchini ili wapewe mafunzo ya pamoja na kwamba vituo vikuu vya kijeshi vitafanyiwa mabadiliko ili kuwakilisha Koo mbalimbali za Somalia.

Mnamo mwezi Machi baraza la Usalama la Umoja wa Matifa lililegeza masharti ya kuuza silaha kwa Somalia na hivyo kuondoa marufuku ya miaka 20 iliyowekwa kuzuia uuzaji wa silaha kwa wababe wa kivita nchini humo.

Waziri Fiqi alisema anatumaini mkutano wa London kwa ajili ya Somalia hapo Mei 7 utaunga mkono Somalia kifedha na katika ngazi nyingine, ikiwa ni pamoja na kusaidia katika ujenzi mpya wa Somalia pamoja na jeshi lake la kitaifa ili kutoa ulinzi wa kutosha ndani ya nchi.

Vikosi vya Umoja wa Afrika kwa ushirikiano na vile vya Somalia na za kikanda zimesaidia kutimua wanagambo wa al-Shabab nje ya miji muhimu ya Somalia, lakini wanamgambo hao wangali wanadhibiti miji midogo na vijiji hususan kusini mwa nchi.

Ethiopia ambayo ina majeshi yake Somalia imeashiria kuchoshwa na hali ya kutokuwa na jeshi thabiti la Somalia. Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn alilimbia bunge wiki jana kuwa ana azma kuu kuondoa majeshi yake Somalia mara tu vikosi vya Somalia na Umoja wa Afrika vitakapochukua jukumu hilo.

Somalia imetaabishwa na miongo mingi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe bila kuwa na serikali kuu hadi pale serikali ya sasa ilipoingia madarakani mwaka jana.
XS
SM
MD
LG