Nchi za mto Nile zinakutana mjini Kampala, Uganda katika hatua ya kuendeleza mazungumzo ya matumizi bora ya maji ya mto Nile. Mkutano huo unahudhuriwa na wajumbe kutoka Tanzania, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Misri, Sudan, Ethiopia, Eritrea, Rwanda, Burundi na Uganda.
Makamu Mwenyekiti wa mazungumzo hayo Wesley Cherchir aliwaambia waandishi wa habari mjini Kampala kuwa nchi nyingine mbili ambazo zimekubali kutia saini mkataba wa kubadili mkataba wa matumizi ya mto Nile wa mwaka 1929.
Wiki iliyopita Makamu Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn alisema katika mahojiano mjini Addis Ababa kuwa nchi za DRC na Burundi karibuni zitatia saini mkataba unaovunja ule wa 1929 ambao ulifikiwa baina ya Misri na wakoloni wa Uingereza.
Mkataba huo uliipa Misri mamlaka ya kura ya veto katika miradi yote inayotumia maji ya Nile, ikiwa na maana kuwa miradi katika nchi ulikoanzia mto na unakopita lazima iidhinishwe na Misri. Katika mkataba mwingine mwaka 1959 Misri na Sudan zilidai matumizi ya asilimia 90 ya maji ya mto huo.
Mwezi Mei mwaka jana mataifa ya Tanzania, Uganda, Kenya, Ethiopia na Rwanda yalitia saini mkataba mwingine kuunda tume itakayosimamia ujenzi wa mabwawa na miradi ya umwagiliaji katika nchi hizo.