Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 25, 2024 Local time: 13:15

Mlipuko mwingine wauwa watu 7 Nairobi


Wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya wakiwa katika moja ya milipuko iliyotokea awali huko Kenya
Wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya wakiwa katika moja ya milipuko iliyotokea awali huko Kenya
Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya linasema takriban watu saba waliuawa na wengine 29 kujeruhiwa katika mlipuko uliotokea kwenye basi ndogo la abiria mjini Nairobi Jumapili.

Mlipuko huo unafuatia mashambulizi kadha ya guruneti katika maeneo mbalimbali ya Kenya yanayotuhumiwa kutekelezwa na wanamgambo wa Somalia wa al-Shabab. Haikubainika mara moja kilichosababisha mlipuko kwenye basi la abiria maarufu kama “Matatu” linalobeba hadi abiria 25 katika mtaa wa Eastleigh mjini Nairobi. Lakini baadhi ya mashahidi na maafisa wa polisi walisema walimwona mtu akilitupia guruneti gari hilo.

Mwandishi wa Sauti ya Amerika-VOA aliyefika mahala pa tukio hilo alisema ilionekana kama mlipuko huo ulisababishwa na bomu la kutengenezwa nyumbani. Mlipuko huo ulikuwa mkubwa kiasi cha kuliteketeza kabisa basi hilo ndogo la abiria.

Shahidi mmoja Mohammed Qadar Gudle alisema alisikia mlipuko huo akiwa umbali wa mita 500 kutoka eneo la tukio hilo. Gudle anasema mapigano yalizuka mara tu baada ya mlipuko huo kwenye mtaa wa Eastleigh na watu wenye hasira wakawageukia na kuwapiga wasomali katika mtaa huo.

Katika miezi ya karibuni Kenya imekabiliwa na mashambulizi ya guruneti katika makanisa na maeneo ya umma yakiwemo mashambulizi mawili ya guruneti katika mtaa huo wa Eastleigh wenye wakaazi wengi wa jamii ya Kisomali.

Polisi wa Kenya wanawalaumu wanamgambo wa al-Shabab kutoka Somalia kwa mashambulizi hayo wakisema kundi hilo linalipiza kisasi kwa mashambulizi ya jeshi la Kenya dhidi ya al-Shabab nchini Somalia .
XS
SM
MD
LG