Mawaziri wa mambo ya nje wa Ufaransa na Ujerumani wametoa wito Ijumaa juu ya Afrika kulaani uvamizi wa Russia nchini Ukraine huku wakishinikiza uhusiano wa kina kati ya Umoja wa Ulaya na nchi mbalimbali barani humo.
"Ni muhimu kukumbuka kwamba kuna mchokozi na aliyeshambuliwa na ni muhimu kila mtu kumwambia mchokozi kwamba lazima aache," waziri wa Ufaransa Catherine Colonna alisema.
"Tuna maslahi ya pamoja na tuna matarajio ya marafiki zetu wa Afrika," Colonna aliwaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa.
Wito huo uliungwa mkono na mwenzake wa Ujerumani Annalena Baerbock ambaye amesema amani barani Ulaya inashambuliwa.
"Tunakuhitaji, tunaihitaji Afrika kutetea amani," alisema Baerbock.
Ukraine na Russia ni wauzaji wakuu wa ngano na nafaka nyingine kwa Afrika, na athari za vita hivyo zimeshuhudiwa kote barani Afrika na ongezeko kubwa la bei ya mafuta, nafaka na mbolea.
Lakini mataifa mengi ya Afrika yameonyesha kusita-sita kulaani uvamizi wa Russia.
Mwezi Novemba mwaka jana, nchi nyingi za Afrika zilijizuia kupiga kura katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la kuitaka Russia kulipa fidia kwa vita kwa Ukraine.
Wajumbe wa Paris na Berlin walizungumza katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat wakati wa kuhitimisha ziara yao ya siku mbili nchini Ethiopia.