Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 04:48

Katibu Mkuu wa UN atoa wito hatua zichukuliwe kukabiliana na tishio la hali ya hewa


Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres

Akizungumza kwa njia ya video katika mkutano na waandishi habari wakati wa kuzindua ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani, WMO, juu ya mabadiliko ya hali ya hewa, Guterres amehimiza haja ya kuacha haraka matumizi ya nishati asili na kuanza kutumia nishati mbadala.

Katibu Mkuu huyo ameelezea kwa kina kile kinachochukuliwa kama mpango wa kuiokoa dunia kwa kuanza kutumia nishati mbadala kote duniani badala ya kutumia gesi, mafuta na mkaa.

Amesema ili kuepuka janga la mabadiliko ya hali ya hewa ni lazima kwa binadamu kukomesha matumizi ya nishati yanayosababisha uchafuzi wa hewa na kuharakisha mpito kuelekea nishati mbadala kabla hatujateketeza nyumba zetu.

Guterres ameongeza kuwa: “Mfumo wa nishati duniani umevunjika, na kutufikisha karibu zaidi katika janga la mazingira. Nishati asilia haina mustakbal mzuri kiuchumi na kimazingira. Vita vya Ukraine na athari zake zilizosababisha kupanda bei za nishati ni onyo jingine. Mustakbal endelevu pekee ni nishati mbadala. Hatuna tena muda wa kusubiri.

Ripoti ya Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani, WMO, inaeleza kwamba vigezo vyote vya mabadiliko ya hali ya hewa vimeweka rekodi kwa mwaka 2021, ikionya kwamba mfumo wa nishati duniani unawapeleka binadamu katika janga kubwa.

Petteri Taalas, WMO.
Petteri Taalas, WMO.

Mkuu wa WMO Petteri Taalas, anasema tuna shuhudia maendeleo mabaya zaidi yatakayoweza kuiangamiza dunia.

Katibu Mkuu wa WMO amefafanua haya: “cha kushtusha zaidi ni kwamba kwa mara nyingine tumevunja rekodi katika kuongezeka gesi za sumu za Greenhouse, yaani Carbon dioxide, methane na nitrous oxide. Tumeshuhudia kuongezeka kwa tindikali baharini, tumeshuhudia kupanda kwa kiwango maji katika kutokana na kuyayuka kwa theluji. Tumevunja rekodi ya joto kikanda.”

Ripoti hiyo iliyopewa jina la Hali ya hali ya hewa duniani kwa 2021, inathibitisha kwamba miaka 7 iliyopita ndio ilikuwa ya joto kali sana kuwahi kutokea, ambapo mfano Ulaya ilishuhudia joto kufikia nyuzi joto 48.8 celsius.

Taalas anasema ni lazima hatua zichukuliwe kwa haraka sana.

Taalas amesema: “Ni muhimu tutangaze juu ya sayansi ya hali ya hewa kwa wananchi, na ingawa vichwa vyote vya habari vinazingatia Ukraine lakini mabadiliko ya hali ya hewa ni hatari zaidi kwa uhai wa binadamu. Na tusipochukua hatua tunaweza kuona athari kubwa zaidi kwa uhai wa binadamu.”

Ripoti inasisitiza juu ya haja ya kuwekeza katika teknolojia zilizo nzuri zaidi kwa mazingira badala ya kuishi na athari za mabadiliko ya hali ya hewa ambazo zitakuwa na gharama kubwa ikiwa hatua hazichukuliwi.

XS
SM
MD
LG