Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Aprili 15, 2024 Local time: 08:14

Idadi ya wakimbizi yaongezeka duniani


Wakimbizi wa Sudan Kusini
Wakimbizi wa Sudan Kusini

Amnesty International yataja DRC, Ivory Coast, Sudan na Sudan Kusini kuwa miongoni mwa nchi zinazokiuka haki za binadamu.

Ripoti ya kila mwaka ya shirika la kutetea haki za binadamu, Amnesty International, inaelezea jinsi idadi ya wakimbizi imeongezeka kote duniani na jinsi jamii ya kimataifa imeshindwa kuwasaidia, hili likiwa mojawapo ya swala kuu la haki za binadamu kwa muda wa mwaka mmoja uliopita.

Shirika hili lenye makao ya London, limeelezea mtandao wa internet kama kifaa muhimu cha kupigana dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu. Amnesty International inasema idadi ya wakimbizi iliongezeka na kufikia milioni 15 mwaka jana huku mamilioni ya wengine wakitoroshwa manyumbani mwao na kuhamia sehemu nyingine za nchi zao ambapo wanaishi kwenye kambi.

Hali hiyo yaripotiwa kuzorota zaidi barani Afrika hususan katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Ivory Coast, Sudan na Sudan Kusini. Lakini kando na nchi zinazokiuka haki za binadamu na kusababisha raia kukimbia, Amnesty International pia linashtumu nchi zinazopokea wakimbizi hao kwa kushindwa kuwasadia inavyopaswa.

Salil Shetty, katibu mkuu wa shirika hilo aliiambia Sauti ya Amerika kuwa serikali husika zinazopokea wakimbizi hutoa kipaumbele katika kulinda mipaka yake na maslahi yake ya kitaifa kuliko kulinda haki za binadamu.

Shirika hilo pia lilitoa hati zinazoonyesha mateso na ukandamizaji katika zaidi ya nchi 100 huku 57 zikiwa na wafungwa wa kisiasa. Shetty anasema matumizi ya teknolojia ya mawasiliano kama vile simu za mkononi, kamera za video na mitandao ya kijamii kama Twitter, imesaidia kuonyesha ukatili unaofanywa dhidi ya binadamu.

Alitoa mfano wa kamera za simu za mkononi ambazo zimetumiwa kurekodi mashambulizi ya raia nchini Syria pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu. Amnesty International inasema japo ripoti na kanda hizo hazizuii mashambulizi hayo, zinaonyesha dunia kile ambacho kisingewezekana miaka ya nyuma na huenda zikazuia manyanyaso na ukiukwaji katika siku zijazo .
XS
SM
MD
LG