Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Aprili 14, 2024 Local time: 23:20

Albino Tanzania wapanga kuelimisha watu juu ya haki zao


Watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Tanzania yaani Albino wamekusudia kuzunguka nchini nzima kuendesha kampeni ya kukabiliana na mauaji ambayo yanaendelea kuwaandama mara kwa mara.

Kampeni hiyo iliyopewa jina la Yatosha ambayo pia inaungwa mkono na makundi ya watu mbalimbali ikiwamo wasanii inatarajiwa kuanzia eneo la kaskazini ya nchi ambako idadi kubwa ya mauaji hayo yamekuwa yakiripotiwa.

Kuanzishwa kwa kampeni hiyo kunatokana na kuibuka upya kwa matukio ya mauaji ya Albino ambayo mara hii yanawahusisha pia wanasiasa ambao wamekuwa wakitajwa kuwa nyuma ya vitendo hivyo katika kile kinachoelezwa kuwa mbinu ya kutafuta kura na kupata ushindi kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Mwanamke akishona kofia kuwasaidia albino Tanzania
Mwanamke akishona kofia kuwasaidia albino Tanzania

Akizungumza juu ya kuanzishwa kwa kampeni hiyo balozi wa harakati hizo ambaye pia ni mlemavu wa ngozi Bwana Henry Mdimu alisema kuwa mkazo mkubwa utakaowekwa ni kutoa elimu kwa wananchi. Alisema kuwa walemavu wa ngozi ni watu wa kawaida kama walivyo wengine hivyo dhana kwamba viungo vyao vinaweza kutumika kwa ajili ya kumtajirisha mtu siyo kweli kabisa.

Hivi karibuni watu wawili walemavu wa ngozi waliuawa huko kaskazini akiwemo mtoto mmoja aliyekutwa amezikwa katika msitu mmoja. Kama sehemu ya kukabiliana na vitendo hivyo wiki iliyopita Rais Jakaya Kikwete alisema kuwa serikali yake itachukua hatua madhubiti ya kukabiliana na wauaji hao aliowaita kuwa ni watu wenye kulipaka matope taifa.

Pia aliahidi kukutana wiki hii na walemavu hao wa ngozi kwa ajili ya kujadiliana namna bora ya kukabiliana na wimbi hilo.

Kuhusu kampeni hii bwana Mdimu ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari alisema kuwa anatarajia kupata uungwaji mkono mkubwa na anaamini kuwa jitihada hizi zinaweza kuzaa matunda haraka iwezekanavyo.

Waganga wa kienyeji pamoja na washirikina ndiyo wanaotajwa kuwa nyuma na vitendo vya mauaji hayo yanayoendelea kutikisa katika kanda ya ziwa. Hivi karibuni jeshi la polisi lilitangaza kupiga marafuku vitendo vyote vya upigaji ramli na kuwataka wale wanaoendesha vitendo hivyo kuacha mara moja.

Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Tanzania kuongeza juhudi zake za kukabiliana na mauaji hayo iliyoyaita kuwa ni ya kinyama na yanayopaswa kulaaniwa na kila mtu.

XS
SM
MD
LG