Wananchi wa Senegal walitii wito wa upinzani wa kuwataka kugonga sufuria na kupiga honi za magari yao siku ya Alhamis katika malalamiko ya kufanya kelele kabla ya uchaguzi wa mwezi ujao.
Siku moja baada ya upinzani kusema kuwa utasitisha maandamano ya mitaani na kushiriki katika uchaguzi wa bunge wa Julai 31 watu walienda kwenye baraza za nyumba zao na kugonga vyombo vyao vya jikoni, ishara ya kuonyesha kutoridhika kwao na utaratibu wa uchaguzi pamoja na hali ya maisha ilivyo sasa.
Mivutano imekuwa ikiongezeka katika taifa hilo la Afrika magharibi kabla ya upigaji kura huo, unaoonekana kama mtihani mkuu kwa Rais Macky Sall. Kura hiyo ni kwa ajili ya bunge la kitaifa lenye viti 165 ambapo wafuasi wa Sall wana wingi wa kura.
Wakati huo huo watu watatu walikufa katika maandamano yaliyositishwa hapo Juni 17 kulingana na takwimu za upinzani na viongozi walipiga marufuku maandamano mengine yaliyoitishwa na upinzani siku ya Jumatano.