Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Julai 14, 2024 Local time: 13:21

Idhaa ya Kiswahili yaadhimisha miaka 60 ya Matangazo


Dr. Aleck Che Mponda mmoja kati ya watangazaji wa mwanzo wa VOA Swahili
Dr. Aleck Che Mponda mmoja kati ya watangazaji wa mwanzo wa VOA Swahili

Kwa miaka 60 matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika yamekua yakisikika kote duniani hasa Afrika mashariki na kati.

Hii ilikua idhaa ya kwanza ya lugha ya Kiafrika kuanzisha matangazo kupitia mitambo ya Sauti ya Amerika mjini Washington D.C. Mwezi Mei 1962 kwa matangazo ya dakika thelathini ambayo yalikuwa yamerekodiwa kwenye ukanda.

Kuanzia mwaka 1962, matangazo yaligeuzwa na kufanywa kipindi kilichotangazwa moja kwa moja, kila siku kutoka Washington, kikirudiwa na kuongezewa habari mpya, mara moja kwa siku.

Mwezi Mei, 15 1966, ndipo matangazo hayo yaliongezewa dakika nyingine thelathini na kuwa matangazo ya saa moja kukiwemo muziki uliorekodiwa na vipindi mbalimbali kutokea mjini Monrovia, Liberia.

Na mwaka uliofuata, 1967, Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika ilizindua matangazo ya moja kwa moja kutoka studio zake mjini Washington D.C.

Mnamo miaka ya hivi karibuni idhaa imepanuka na inatangaza kupitia redio, televisheni na mitandao ya kijamii.

Kwa upande wa redio inatangaza kwa saa mbili kwa siku, pamoja na nusu saa ya matangazo ya televisheni ya Duniani Leo.

Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili huwafikia mamilioni ya wasikilizaji katika Afrika Mashariki na Afrika ya kati Pamoja na sehemu nyingine za dunia kupitia ukurasa wetu wa mtandao wa www.voaswahili.com.

Idhaa ilipoanza miaka 60 iliyopita ilikua inatumia mitambo ya masafa mafupi Short Wave, lakini kutokana na kuendelea kwa teknolojia hivi sasa tunatangaza kupitia pia kwenye mitambo ya FM kupitia redio zetu shirika za kanda ya Afrika Mashariki na Kati.

Mbali na matangazo ya moja kwa moja tuna vipindi vya televisheni vya kila wiki vya Afya Yako, Zulia Jekundu na Washingotn Bureau.

VOA Swahili imekua mstari wa mbele katika kutangaza matukio muhimu ya dunia na yanayotokea kanda ya Afrika Mashariki na Kati, katika kila nyanja ya habari.

Wasikilizaji waendelea kushiriki moja kwa moja hasa katika matangazo yetu ya VOA Express kupitia ‘Barazani’ na ‘Swali la Leo’, 'Maswali na Majibu', na 'Salamu Zenu'.

Malengo makuu ya Idhaa ya kiswahili ya Sauti ya Amerika kwa hivi sasa ni kuhakikisha tuna leta usawa wa jinsia kwenye matangazo yetu kwa kuongeza sauti za wanawake, pamoja na kuwashirikisha zaidi vijana.

XS
SM
MD
LG