Wachumi wanabashiri kwamba Kenya ni miongoni mwa nchi zilizoko kwenye hatari ya kuathirika kiuchumi kutokana na Uingereza kutaka kuondoa uanachama wake katika umoja wa ulaya.
Uingereza inatarajiwa kupiga kura Alhamisi ili kuweza kufikia uamuzi wake au la.
Gavana wa benki kuu ya Kenya Patrick Njoroge ambaye ni mchumi wa zamani katika shirika la fedha la IMF anasema uchumi mkubwa wa Afrika mashariki unaweza ukatingishwa pamoja na uchumi katika nchi nyingine duniani kama uingereza itaamua kuondoka katika uanachama huo.
Maelezo ya Dr. Njoroge yanatathminiwa kuonyesha wasiwasi kwamba watunga sera wa uchumi nchini Kenya wanaona kwamba matokeo ya kujitoa uingereza katika umoja wa ulaya yanaweza kusababisha mzozo wa uchumi uliotokea mwaka 2008 duniani.
Kama uingereza itafikia uamuzi wa kujiondoa katika uanachama wa umoja wa ulaya, Nairobi inaweza kutumbukia katika mtikisiko wa kukosa mikopo kutokana na mzozo utakaokuwepo katika masoko ya dunia ambayo yanatarajia kufuata kura ya kujitoa huko.
Watafiti wanasema makampuni ya Kenya yanayosafirisha bidhaa Uingereza pia biashara zao zinaweza kuzorota kama Uingereza itajitoa kwenye umoja wa Ulaya.