Umoja wa Mataifa na mataifa makubwa, yametoa mwito kwa pande zinazopingana nchini Libya, kufikia makubaliano ya kugawana madaraka ili kumaliza mapigano ya karibu mwaka wa nne, ugaidi na hali tete ya kisiasa.
Mwanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa, na maafisa wengine wa ngazi ya juu wamekutana Berlin, Ujerumani, jana Jumatano, na kutoa taarifa ya pamoja kwamba kumaliza mgogoro wa kisiasa ndio suluhisho pekee la matatizo ya Libya.
Wamewataka Walibya wote kuondoa vikwazo vilivyo salia kufanikisha mpango huo.
Karibu wawakilishi 20 wa Libya, walikuwepo Berlin, kwa mazungumzo ambayo yalijumuisha wanadiplomasia kutoka wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama, la Umoja wa Mataifa, ambao ni Uingereza, China, Ufaransa, Russia na Marekani, ambapo pia Umoja wa Ulaya, Italia, Spain na majirani wa Libya kutoka Afika Kaskazini walihudhuria.