Maafisa wa usalama wa Ufaransa wanajadiliana na ndugu wawili wenye silaha wanaodhaniwa walihusika na shambulizi la kigaidi lililosababisha vifo vya watu 12 katika ofisi za jarida la Charlie Hebdo, siku ya Jumatano.
Said na Cherif Kouachi wanaripotiwa waliwambia maafisa wa polisi wanaozungumza nao kwamba wako tayari kufariki kama mashuja, kuliko kujisalimisha.
Msako mkubwa wa polisi ukisaidiwa na helikopta, magari ya polisi na ya zima moto umefika katika mtaa wa viwanda wa Dammartin-en-Goele, karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Charles DeGaulle karibu kilomita 40 kaskazini mashariki ya Paris.
Polisi wanathibitisha kwamba ndugu hao wanawashikilia mtu mmoja mateka, lakini hwanahabari ikiwa kuna watu wengine wanaoshikiliwa na njia zote za kuingia na kutoka mji huo zimefungwa na wakazi wameombwa kubaki ndani.
Watu tisa wanashikiliwa hadi sasa kuhojiwa kuhusiana na shambulizi la jumatano. zaidi ya polisi na maafisa wa usalama elfu 88 wamekuwa wakiwatafuta ndugu hao wawili walokimbilia maeneo ya kaskazini ya Paris.