Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Julai 25, 2024 Local time: 16:50

Marekani yaadhimisha mwezi wa Historia ya Watu Weusi.


Martin Luther King Jr akihutubia miaka 47 iliyopita.
Martin Luther King Jr akihutubia miaka 47 iliyopita.
Desturi moja ya kukukmbuka na kusherehekea matukio muhimu katika
historia ya watu wenye asili ya Kiafrika kila mwaka, hufanyika mwezi wa pili hapa Marekani

Hiyo desturi ilianzishwa mwaka 1926 na mwanahistoria mweusi na mashuhuri sana, Dkt. Carter G. Woodson, akiungwa mkono na Shirikisho la Uchunguzi wa Historia na Maisha ya Mnigro (Association for the Study of Negro Life and History) .

please wait

No media source currently available

0:00 0:41:35 0:00
Kiungo cha moja kwa moja

Hapo awali, ukumbusho huo ulifanyika kila mwaka kwa muda wa
juma moja tu sio kwa mwezi mzima kama ulivyo sasa hivi. Wiki ya pili
ya mwezi wa pili, yaani mwezi wa Februari, ilichaguliwa kwa sababu
ndipo mwezi walipozaliwa Frederick Douglass na Rais Abraham
Lincoln.

Douglass alikuwa mtumwa mtoro ambaye alijaaliwa akili kali
kama wembe na licha ya hilo pia akawa na kipaji cha ufasaha wa
lugha. Yeye alipinga vikali utumwa nchini Marekani.

Abraham Lincoln alikuwa rais wa 16 wa Marekani naye akashika
uongozi wa nchi wakati wa hatari wa vita vya wenyewe kwa
wenyewe, ikawa kipindi cha ghasia na machafuko kilichohatarisha
uwezo wa Marekani kubaki kama nchi moja. Lincoln vilevile akapinga
utumwa na ndiye aliyewaachilia huru watumwa weusi.

Upanuzi wa Black History Week hadi ikawa mwezi mzima
ulipendekezwa mwaka 1969 na viongozi wa wanafunzi weusi wa chuo
kikuu cha Kent State huko jimboni Ohio. Mwaka mmoja baada ya
pendekezo hilo kutolewa (yaani1970) Black History Month
ikasherehekewa mwezi wa pili kwa mwezi mzima kuko huko chuoni
Kent State.

Mwaka wa 1976 Marekani ilisherehekea miaka 200 tangu
ilipata, kwa kunyanyua silaha za vita, uhuru wake kutoka
Uingereza. Mwaka huohuo aliyekuwa rais wa Marekani, Gerald Ford,
akawahimiza Wamarekani wote, wazungu kwa weusi, ya kwamba
wasisahau michango kemkem iliyotolewa na wananchi weusi katika
ukuaji na maendeleo ya nchi hii tangu mwanzo.

Mwaka 1987 ndio mwaka wa kwanza wananchi wa Uingereza, nchi
yenye raia wengi wenye asili ya Kiafrika, walipoanza kusherehekea
Black History Month kwao.

Mwaka wa 1995, serikali ya Canada, nchi nyingine yenye wananchi
chungu nzima wenye asili ya Kiafrika, ilipitisha muswada bungeni pao
kwamba mwezi wa pili nao pia utakuwa mwezi rasmi wa Black History
Month.

Historia ya Waafrika nchini Marekani ni historia ndefu. Ni historia
iliyoanza kabla Marekani haijawa nchi kamili na huru yenye jina hilo la
Marekani. Yaani, nchi inayoitwa leo Marekani, katika karne ya 17
ilikuwa mkusanyiko wa makoloni kumi na matatu yaliyokuwa chini ya
utawala wa Uingereza.

Vilevile ni historia ya watu ambao mwanzoni waliitwa Waafrika lakini,
baada ya muda kupita, watu hao hao wakabadilishiwa jina wakawa
Wanigro au “watu wa rangirangi.” Enzi ya leo watu hao hao pengine
waitwa Waafrika wa Marekani, na pengine waitwa watu wenye asili ya
Kiafrika, au mara nyingi zaidi, huitwa tu Wamarekani weusi.

Linginelo la kuzingatiwa ni kwamba Waafrika wa kwanza walioletwa
Marekani, mwanzoni si wote hao walikuwa watumwa, hata kidogo.
Wengine walikuwa watumishi kwa muda fulani huku wengine
wakawa watumwa halisi. Hata hivyo, haikuchukua punde ngozi
nyeusi ikawa alama thabiti ya utumwa na yule mwenye ngozi hiyo
hana budi awe mtumwa.

Historia ya weusi nchini Marekani, kama ilivyotangulia kutajwa, ni
ndefu lakini licha ya hilo pia ni ya kusisimua. Ni historia ya mgongano
baina ya wema na ubaya na vilevile mgongano baina ya nguvu za
kisiasa, za kiuchumi, za kidini, na za kijamii zikikinzana.

Twaelewa fika kuwa utumwa umekuweko katika takriban nchi zote
duniani tangu zama za asili na jadi. Kwa mfano, utumwa ulikuwako
Misri ya kale, Uyunani, na Dola ya Roma. Ulikuwa pia (pengine bado
uko hapa na pale) Uchina, Uarabuni, barani Afrika, Ulaya, na
kwingeneko.Hapo hakuna mabishano. Vilevile hakuna mabishano
ya kuwa utumwa popote pale ulipokuwa na ulipo ni kitu kiovu. Lakini
ukweli huu haumaanishi kwamba utumwa mahali fulani ni sawasawa
na utumwa pahala pengine. Mathalan, tukilinganisha utumwa
uliokuwa nchini Marekani na ule uliokuwa Uarabuni, japo mifumo
yote miwili ilimnyima aliyetiwa utumwani uhuru wake, kulikuwa na
tofauti fulani fulani kati yao pia.

Kwa mfano, huko Uarabuni ilikuwa si haba kumwona mtu ambaye
hakuwa Mwislamu wakati alipotiwa utumwani, akislimu mara nyingi
huyo huyo aliweza kuachiliwa, ama papo hapo au wakati fulani siku
za usoni. Hata ukawa uwezekano ya kwamba yule mtumwa
aliyeachiliwa, ingedhihirika kuwa huyo ametunukiwa vipaji adimu
kama vile akili ya kuchata, hekima, na ujasiri, angeweza kupewa
hadhi kubwa kijamii.

Nchini Marekani mambo yalikuwa vingine kabisa. Mamilioni ya
Waafrika, waliokubali dini ya Ukristo au walikuwa Wakristo tangu
kuzaliwa, lakini hadhi yao ikabaki vilevile, hususan pande za kusini
mwa nchi. Na Mwafrika aliyebahatika kupewa uhuru wake kwa
sababu moja au nyingine, au kama Mwafrika fulani alirehemiwa
kuweza kujinunulia uhuru wake, kwa mtu wa namna hiyo kushika
cheo kikubwa cha kijamii ingekuwa jambo la muhali mithili ya
kuona paka mweusi katika giza la usiku.

Tofauti nyingine baina ya mifumo hiyo miwili ya utumwa ni kwamba
Mwarabu angemshikisha mimba kijakazi au suria wake, kama yule
mtoto atakayezaliwa aghalabu huzaliwa huru, na hasa hasa ikiwa
mtoto huyo ni wa kiume. Ndiyo kusema, kwa kawaida hakukuwa na
watumwa aina ya “Chicken Jorji” miongoni mwa Waarabu waliokuwa
Waislamu.

Huko Marekani enzi za utumwa mambo yakawa vingine. Mabwana
wengi wenye watumwa (sio wote lakini wengi), kila uchao, hawakuwa
na shida yoyote ya kuwaangalia watoto wenye damu yao
wakimenyeka mashambani pao kuanzia mapambazuko hadi mchweo,
siku nenda siku rudi, mara nyingi wakichomwa na miale ya jua kali,
kupigwa na mvua, au kuumwa na nyoka na mbu.

Namalizia hapa kwa kurudia kauli niliyotamka hapo juu ya kuwa
utumwa ni utumwa wala hakuna utumwa ulio mzuri. Utumwa ni mwovu mtupu po pote ulipo.
Makala haya ni mchango wa Profesa John Mtembezi Inniss.
XS
SM
MD
LG