Miili ya wanajeshi saba wa Tanzania waliokuwa katika kazi za kutekeleza ulinzi wa amani wa kimataifa katika mkoa wa Darfur nchini Sudan imewasili leo na ndege maalumu ya Umoja wa Mataifa.
Wanajeshi hao waliuwawa mwezi Julai, kufuatia shambulizi la ghafla wakiwa nchini Sudan.
Kaimu mkurugenzi wa habari wa JWTZ, Meja Joseph Masanja amesema miili hiyo imewasili Jumamosi majira ya saa kumi kasorobo katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu J. K. Nyerere na imehifadhiwa katika hospitali ya jeshi ya Lugalo hadi Julai 22 ambapo itaagwa rasmi.
Shughuli za kuagwa miili hiyo zitafanyika katika viwanja vya wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga taifa vilivyoko Upanga jijini Dar es salaam.