Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 08:15

Wafanyakazi wa mashirika yasiyo ya serikali Uganda waandamana kupinga ufisadi.


Rais Museveni akizungumza na waandishi.
Rais Museveni akizungumza na waandishi.
Wafanyakazi wa mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Uganda wameandamana Jumatatu wakipinga kiwango cha ufisadi ambacho wanasema kimepita kiasi nchini humo .

Ofisi zote za mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Uganda zilifungwa mchana kutwa. Mamia ya wafanyakazi wa mashirika haya wakiwa wamevalia nguo nyeusi walikusanyika kwenye lango kuu la uwanja wa maonyesho ya kilimo mjini Kampala.

Watu hao walisema wanaomboleza kifo cha nchi yao ambayo kwa wakati mmoja iliitwa “Lulu ya Afrika”. Wanasema ufisadi umeimaliza nchi yao na ndio sababu wiki hii yote itakuwa wiki ya kuomboleza ufisadi ambao umekita mizizi serikalini pamoja na kuwashinikiza wananchi waamke na kuungana nao kuishinikiza serikali kuwafukuza kazi maafisa wote ambao wametajwa kwenye kesi za ufisadi.

Miria Matembe ni mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu na kwa wakati fulani alikuwa waziri wa maadili kwenye serikali ya rais Museveni.

“Hatutaendelea kuibiwa rasili mali yetu tuliyopewa na mwenyezi Mungu na kuongozwa na watu ambao wanawalinda wezi. Hatutakubali. Tunataka kuwaambia watu wawache kuogopa. Mimi nilikuwa hapa wakati wa utawala wa Idi Amin. Pindi watu walipozidi kuogopa, serikali ya Amin iliendelea kuwakandamiza na hata wengine kuuliwa. Wakati umefika wa Uganda kuacha kuogopa. Wacheni kuogopa”.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na muungano wa mashirika yasiyo ya serikali, serikali imepoteza dola za Marekani milioni 400 kupitia ufisadi.

Ofisi ya waziri mkuu imekuwa ikitajwa sana kwenye sakata ya wizi wa dola zipatazo milioni tisa zilizofaa kuwasaidia wakazi wa kaskazini mwa nchi ambao wameathiriwa sana na vita vya LRA. Sakata hii imewalazimu baadhi ya wafadhili kukata misaada wanayoipa serikali ya Uganda.

Wengine wanaotajwa kwenye kesi za ufisadi ni mke wa rais Museveni, mama Janet Museveni ambaye anasemekana alibadilisha pesa alipokwenda nchini Israel mara nane kwenye kipindi cha mwezi mmoja.

Ingawa Bi. Museveni ambaye ni waziri wa eneo la Karamoja anasema hakwenda Israeli, baadhi ya wakinamama waliondamana Jumatatu walililia wakisema itakuwa bora akiondoka serikalini na arudi nyumbani ampikie mumewe.

Mashirika yasio ya kiserikali yanapanga kuvitembelea vijiji vyote nchini Uganda na kuwaonyesha watu michezo ya kuigiza kama njia moja ya kuwaelemisha jinsi ufisadi unavyofanyika serikalini na jinsi wanafaa kukabiliana na watu wanaotajwa kwenye kesi za ufisadi. Pia wanawataka wananchi kutowaalika maafisa mafisadi wa serikali kwenye mikutano yao kama vile harusi na harambee kwa sababu pesa wanazochanga ni za wizi.
XS
SM
MD
LG