Maafisa wa idara ya kijasusi wa Marekani wametoa ripoti ya kina kuhusu kilichotokea katika shambulizi la mauaji kwenye ubalozi wa Marekani mjini Benghazi, Libya katika kujibu shutuma kwamba hakukuwa na hatua za kutosha zilizochukuliwa kuzuiya shambulizi hilo.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotambulishwa maafisa wa ngazi za juu wa ujasusi waliwaambia waandishi wa habari siku ya ijumaa kwamba CIA ilipeleka kundi la uokozi katika kituo cha karibu cha jeshi ndani ya dakika 25 walipotaarifiwa kuhusu shambulizi hilo lililomuuwa balozi wa Libya na wamarekani wengine watatu.
Lakini amesema kundi hilo lenye wajumbe sita halikuwasili hadi dakika 25 baada ya tukio, kwa sababu ya kushindwa kupata msaada kutoka kwa wanamgambo wa Libya wakiwa na silaha nzito na pia kwa sababu walishambuliwa wakati walipokuwa wanawasili kwenye ubalozi huo.
Maafisa wa CIA wameripoti kwamba walibaki ndani ya ubalozi huo kwa muda wa saa moja kabla ya kuondoka na wamarekani wote isipokuwa balozi ambae alikuwa amechukuliwa kupelekwa kwenye hospitali ya karibu na eneo la shambulizi.