Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 25, 2024 Local time: 10:34

Marekani kukabidhi mpango wa ARV kwa Afrika kusini


Hillary Clinton
Hillary Clinton
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton anasema Washington imeanza kuhamisha mpango unaodhibiti dawa za kupunguza kasi ya maambukizo ya ukimwi kwenda Afrika Kusini ambayo ina kiwango kikubwa cha maambukizo ya HIV duniani.

Clinton alitoa matamshi hayo Jumatano wakati akihutubia kwenye chuo kikuu cha Western Cape kilichopo nje ya Cape Town. Alisema makubaliano hayo ni hatua moja kubwa nchini Afrika Kusini katika mapambano dhidi ya virusi hivyo.

Marekani ilidhibiti njia za utoaji msaada wa fedha za HIV na ukimwi kwenda kwenye serikali ya Afrika Kusini wakati wa utawala wa Rais wa zamani wa nchi hiyo Thabo Mbeki ambaye alikataa kwamba kulikuwa na uhusiano kati ya HIV na ukimwi na alikataa tiba iliyotambulika kimataifa kwa ajili ya ugonjwa huu.

Washington imetumia dola bilioni 3.2 tangu mwaka 2004 kwa ajili ya program ya HIV na ukimwi nchini Afrika Kusini. Japokuwa nchi hiyo imepiga hatua katika kupunguza kiwango cha maambukizo zaidi ya asilimia 17 ya watu nchini humo wana virusi vya HIV.

Clinton ambaye yupo kwenye ziara yake ya siku nne nchini humo alikutana Jumanne na maafisa waandamizi wa Afrika Kusini katika mji mkuu wa Pretoria ambao unataka ushirikiano mkubwa kati ya Afrika Kusini na Marekani.

Kundi la Human Rights Watch Jumatano lilimtaka Clinton kumshinikiza Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan kushughulikia ghasia zinazoongezeka huko kaskazini na kati kati mwa Nigeria wakati atakapoitembelea nchi hiyo wiki hii.

Kundi hilo lilisema ghasia nyingi zimekuwa zikifanywa na kundi la waislam wenye msimamo mkali la Boko Haram. Lakini pia linasema majeshi ya usalama ya Nigeria yamewakamata mamia ya watu na kuwaweka kizuizini bila ya kuwafungulia mashtaka au kuwafikisha mahakamani.
XS
SM
MD
LG