Waliopoteza makazi Kenya hawajaridhishwa na malipo ya serikali

Kambi ya watu walopoteza makazi yao baada ya uchaguzi wa 2007 kwenye uwanja wa Afraha, Nakuru

Wakenya walopoteza makazi yao wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 wanasema wameridhika na hatua ya haraka ya serikali ya Kenya kuwalipa fidia, lakini wanadai fedha haitawatosha kuanzisha upya maisha yao.

Akizungumza na sauti ya Amerika, mwenyekiti ya umoja wa watu walopoteza makazi yao Kenya Steven Mmbugwa ameipongeza serikali mpya ya Uhuru Kenyatta kwa kushughulikia haraka madai yao lakini anasema "serikali iliyopita ilikua inanunuwa mashamba mahali ambapo wa IDP's hawakufurahishwa nayo. Ingawaji kwa maoni yetu tunaona hatua hii mpya ni nzuri lakini fedha serikali itatoa hazitoshi kununua mashamba kuweza kukidhi mahitaji yao."

Your browser doesn’t support HTML5

Mahojiano na Steven Mmbugwa


Wakazi hao wanataka serikali kuwapatia angalau shilingi milioni moja kuweza kununua eka mbili za shamba kama walivyokubaliana awali, na kuweza kuanza kilimo na maisha mepya.

Kwa upande mwengine Bw. Mmbugwa, anasema wanapanga maandamano ya kitaifa hapo Septemba 15 kudai kufutiliwa mbali kesi dhidi ya wakenya wanne akiwemo rais na makamu rais mbele ya Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa, ICC, kutokana na ushahidi usoaminika.