Waasi wa Yemen na vikosi vya serikali wamewaachilia huru wafungwa kwa mabadilishano

Mpatanishi wa Yemen, Yasser al-Haddi (chini) akionyesha ishara ya amani wakati wa mabadilishano ya wafungwa na waasi wa ki-Houthi wenye makao yao Sanaa, Yemen. April 14, 2023

Ndege tano zilizowabeba karibu wafungwa 200 kutoka pande zote mbili ziliruka kati ya mji mkuu wa Sanaa unaodhibitiwa na waasi wa ki-Houthi na mji wa kaskazini wa Marib unaodhibitiwa na serikali

Waasi wa Yemen na vikosi vya serikali waliwaachilia huru wafungwa kadhaa Jumapili akiwemo mwanamke katika mabadilishano ya mwisho ya siku tatu ya karibu wafungwa 900 na kuongeza matumaini ya kumaliza vita vyao vya muda mrefu.

Ndege tano zilizowabeba karibu wafungwa 200 kutoka pande zote mbili ziliruka kati ya mji mkuu wa Sanaa unaodhibitiwa na waasi wa ki-Houthi na mji wa kaskazini wa Marib unaodhibitiwa na serikali. Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imesema idadi ya wafungwa walioachiliwa huru kwa siku tatu inafikia 869 chini ya makubaliano yaliyofikiwa nchini Uswisi mwezi uliopita.

Miongoni mwa waliobadilishana siku ya Jumapili ni mwanamke mmoja Samira Machi ambaye vikosi vya serikali vilimkamata miaka mitano iliyopita kwa kutuhumiwa kuandaa milipuko iliyosababisha vifo vya watu kadhaa alisema afisa wa serikali kwa sharti la kutotajwa jina.

Aliachiliwa huru kwa kubadilishana na pia kuachiliwa kwa waandishi wa habari wanaoshikiliwa na Wa-houthi mpatanishi wa serikali Majed Fadail alithibitishia kwa shirika la habari la AFP. Waandishi hao wanne walikuwa wamehukumiwa kifo na Wa-houthi wanaoungwa mkono na Iran.