Uchaguzi mkuu wa Rwanda kufanyika Julai mwaka ujao

Rais wa Rwanda Paul Kagame.

Tume ya uchaguzi ya Rwanda imesema Jumanne kwamba uchaguzi wa Rais na bunge utafanyika Julai 15 mwaka ujao, wakati rais Paul Kagame akiwania kwa mhula wa nne.

Tume hiyo kupitia ujumbe wa X imesema kwamba uchaguzi wa rais pamoja na wajumbe 53 waliochaguliwa na vyama vya kisiasa, au wagombea huru utafanyika Julai 15, 2024. Kagame mwenye umri wa miaka 66 ametawala taifa hilo lisilo pakana na bandari kwa karibu miongo minne.

Mwaka 2015 alisimamia marekebisho yenye utata ya katiba, yaliomuruhusu kuwania kwa mihula zaidi, na kumuwezesha kuwa madarakani hadi 2034. Kagame ambaye alikuwa kiongozi wa waasi alichaguliwa kuwa rais wa taifa hilo kupitia uchaguzi wa kwanza mwaka 2000, ingawa amekuwa kiongozi wa taifa hilo tangu kumalizika kwa mauaji ya kimbari ya 1994.