Raia wa Gambia wanapiga kura Jumamosi kumchagua rais ajaye nchini humo

Rais Adama Barrow wa Gambia

Rais Barrow anawania kuchaguliwa tena kwa muhula mwingine madarakani, lakini pia Yahya Jammeh aliye uhamishoni bado anaushawishi mkubwa kisiasa kwa wananchi wake nchini humo katika kampeni za urais zinazomalizika Ijumaa

Wananchi wa Gambia watapiga kura Jumamosi kumchagua rais, katika uchaguzi wa kwanza wa nchi hiyo maskini ya Afrika magharibi tangu aliyekuwa diktekta Yahya Jammeh kukimbilia uhamishoni takribani miaka mitano iliyopita.

Wapiga kura katika taifa hilo dogo huko Afrika wana wasiwasi kuhusu kuboresha hali ya maisha. Lakini Jammeh ambaye alinyakua mamlaka nchini Gambia mwaka 1994 na kutawala kimabavu kwa miaka 22 bado ana ushawishi mkubwa.

Yahya Jammeh (L) na mkewe Zineb Jammeh

Uwezekano wa kurudi kwake kutoka uhamishoni na jinsi nchi inavyopaswa kujibu mlolongo wa uhalifu unaodaiwa chini ya utawala wake ikiwa ni pamoja na ubakaji, mateso, na kutumia makundi ya mauaji mambo yaliyoidhinishwa na serikali, yamekuwa mada kuu katika kampeni inayomalizika leo. Baadhi ya wananchi wa Gambia wanasema masuala ya kiuchumi ndio yanawatia wasi wasi zaidi.

Kwa Rais Adama Barrow mwenye umri wa miaka 56 ambaye anawania kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi huu ni kama kura ya imani kupima uwezo wake wa kuleta maendeleo.

Kuna wagombea wengine watano wanaoshiriki kwenye uchaguzi huo ingawa mkongwe wa kisiasa Ousainou Darboe mwenye miaka 73 anachukuliwa kuwa mkombea mkuu wa upinzani.