Makamu rais Marekani awahakikishia Poland na Romania uungaji mkono

Makamu Rais wa Marekani Kamala Harris akiwasili katika uwanja wa ndege kwa safari yake kuelekea Poland na Romania kwa ziara ya siku tatu.

 Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris atashirikiana na Poland na Romania kwa hatua zinazofuata za kukabiliana na uvamizi wa Russia dhidi ya Ukraine na kuwahakikishia uungaji mkono wa Washington wakati wa mikutano yake na viongozi wa nchi zote mbili kuanzia Alhamisi.

Nchi hizo zimezidi kupata wasi wasi kuhusu uvamizi wa Russia katika eneo hilo na ni wanachama wa NATO walio mbali zaidi mashariki. Wanashirikiana mpaka na Ukraine, ambapo maelfu ya wakimbizi wanamiminika huko.

Harris ataangazia njia ambazo wanachama wa NATO wanaweza kutekeleza vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na jinsi wanavyoweza kukaa sawa na kusonga mbele pamoja, maafisa wakuu wa utawala walisema.

Pia atawasiliana na wakimbizi wa Ukraine nchini Poland, kujadili kuendelea kwa misaada ya kibinadamu na usalama kwa Ukraine na eneo hilo, walisema. Idadi ya wakimbizi waliotokana na uvamizi huo imevuka milioni 2.