Mashambulizi hayo yametokea wakati maafisa wa Israel wakisubiri ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, ambaye amesema kwamba ataomba Israel ijiepushe na mauaji ya raia kwenye operesheni zake huko Gaza, pamoja na kufanikisha upelekeji misaada kwa raia wa Palestina.
Blinken pia ameelezea wasi wasi wake kuhusu uwezekano wa kusambaa kieneo kwa ghasia hizo. “Huu ni mzozo unaoweza kuenea na kusababisha ukosefu zaidi wa usalama, pamoja na mateso,” Blinken amesema Jumapili. Hata hivyo waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kuendelea na mapigano, wakati akiwa kwenye kikao cha kila wiki na baraza lake la mawaziri hapo Jumapili.
Wakati wa kikao hicho, Netanyahu alisema kwamba. “Ni lazima vita viendelee hadi tufikie malengo yetu ya kuiangamiza Hamas, pamoja na kuachiliwa kwa mateka wote, huku tukihakikisha kwamba kundi hilo halitokuwa tena tishio kwa Israel.”