Cameroon yapokea shehena ya chanjo za Malaria kutoka Uingereza

Picha ya muuguzi akitayarisha sindano yenye chanjo ya Malaria. Picha ya maktaba.

Cameroon Jumanne jioni imepokea shehena ya kwanza ya chanjo za Malaria aina ya Mosquirix kutoka katika kampuni ya kutengeneza dawa ya Uingereza ya GSK Plc, wakati taifa hilo likikabiliana na ugonjwa huo unaoua zaidi ya watu 600,000 kila mwaka kote ulimwenguni.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, shehena ya chanjo 331,200 zinazojulikana pia kama RTS, S, ziliwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Nsimalen mjini Yaounde, ikiwa ya kwanza kwa mataifa ya kiafrika, baada ya program za majaribio kufanyika Kenya, Ghana na Malawi.

Shirika la afya duniani WHO limesema kwamba Malaria bado ni ugonjwa hatari zaidi barani Afrika, wakati ukiua karibu watoto nusu milioni waliopo chini ya umri wa miaka 5 kila mwaka, na kuchangia asilimia 95 ya jumla ya maambukizi ya malaria kote ulimwenguni, kufikia 2021.

Shehena ya kwanza ya chanjo iliyowasili Cameroon itasambazwa miongoni mwa vituo 42 vya afya, kati ya 203 vilivyolengwa kote nchini, amesema waziri wa afya Manaouda Malachie.