Kundi la Islamic State limedai kuhusika na shambulizi la DRC lililouwa watu 15

Wanamgambo wa Islamic State katika picha iliyotolewa March 29, 2021 katika mji wa Palma nchini Msumbiji

Islamic State siku ya Jumanne lilidai kuhusika na shambulizi lililoua takribani raia 15 katika kijiji kimoja kaskazini-mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo siku ya Jumapili. Kundi hilo la wanamgambo lilisema kwenye mtandao wake wa mawasiliano ya telegram.

Kundi la kutetea haki za binadamu na afisa mmoja wa eneo hilo alisema Jumatatu kwamba wapiganaji wanaoaminika kuwa wanachama wa Allied Democratic Forces (ADF) walivamia kijiji cha Bulongo katika jimbo la Kivu kaskazini, baada ya kiza kuingia siku ya Jumapili na kuharibu nyumba pamoja na kuwaua wakaazi ambapo walipita kwenye njia yao na kuchoma moto magari sita.

ADF ni wanamgambo wa Uganda ambao wamekuwa wakiendesha harakati zao mashariki mwa Congo tangu miaka ya 1990 na kuua raia wengi ambapo wengi wao ni katika mashambulizi ya usiku wa manane yaliyofanywa kwa kutumia mapanga na mashoka.

Pia kundi liliahidi ushirika na Islamic State mwaka 2019. Islamic State ilidai kuwa wanachama wake waliwauwa takribani wakristo 20 na kuchoma moto malori sita katika shambulizi hilo kwa kutumia bunduki za rashasha na kurejea katika vituo vyao bila kuumia.