Ghasia zazuka wakati wa kura ya maoni Misri.

Wanawake wakiwa wamepanga foleni kupiga kura.

Raia wa Misri wanaendelea kupiga kura Jumatano ikiwa ni siku ya mwisho ya kushiriki katika kura ya maoni , kuamua kama wataidhinisha katiba mpya ya serikali ya mpito inayoungwa mkono na jeshi.

Kura hiyo ya maoni ni sehemu ya mpango wa mpito wa kisiasa uliotangazwa baada ya kutimuliwa madarakani rais wa zamani Mohamed Morsi Julai mwaka jana. Kama itapitishwa kura ya maoni ya katiba itafuatiwa na uchaguzi mpya wa rais na bunge.

Maelfu kwa maelfu ya Polisi na wanajeshi wamesambazwa kote nchini kuimarisha ulinzi lakini ghasia baina ya wafuasi na wapinzani wa bwana Morsi zimesababisha takriban vifo vya watu nane. Kundi la Muslim Brotherhood linalomuunga mkono Morsi limewahimiza wamisri kususia zoezi hilo likidai linakwenda kinyume cha sheria.