Rais mpya wa Zambia Michael Sata amesema taifa hilo litaongozwa kwa kuzingatia amri kumi za Mungu kama ilivyoagizwa katika Biblia. Rais Sata alisisitiza zaidi mojawapo ya amri hiyo inayosema ‘ hutaiba’ alipotoa hotuba yake katika kanisa moja ya Roman Katoliki mjini Lusaka Jumapili. Rais huyo ambaye ni muumini wa dini ya Roman katoliki amesema serikali yake itakuwa na ushirika wa karibu na Kanisa. Bwana Sata aliapiashwa Ijumaa baada ya kushinda uchaguzi wa urais dhidi ya rais Rupiah Banda na kuahidi kupigana vikali na ufisadi na kusaidia raia maskini wa Zambia. Zambia ina waumini wengi wa dini ya Kikristo ingawa watu milioni 14 wanafuata imani ya Kihindu, Kiislam na dini za kijadi. Katiba ya Zambia inasema taifa hilo ni la Kikristo na kwamba litaheshimu haki za raia wote na kuwapa uhuru wa kidini.
Rais mpya wa Zambia asema ataongoza kwa kufuata Biblia