Moja ya vyama vikuu vya wafanyakazi nchini Afrika Kusini kimekataa pendekezo jipya la nyongeza ya mishahara kutoka kwa serikali ili kumaliza mgomo wa wiki mbili.
Chama chenye wanachama laki 2 cha National Education Health and Allied workers kimekataa pendekezo hilo baada ya mazungumzo na wawakilishi wa serikali Jumatano. Makundi mengine hayajatangaza uamuzi wao.
Lakini pendekezo hilo jipya la serikali limepelekea chama cha wafanyakazi wa migodi kuacha mgomo uliokuwa umepangwa kufanyika Alhamis. Chama hicho cha wafanyakazi kilisema kimesitisha mgomo huo ili kuwapa wafanyakazi wa serikali muda wa kufanya maamuzi mapya juu ya pendekezo hilo.
Pendekezo jipya la serikali lilikuwa la kuongeza mshahara kwa asilimia 7.5 na marupurupu ya nyumba ya dola 109. Vyama vya wafanyakazi wa umma vilidai nyongez ya asilimia 8.6 na pamoja na posho la nyumba.
Mgomo huo wa wafanyakazi wa umma wapatao milioni 1.3 umepelekea kufungwa kwa shule na wanajeshi kuagizwa kuchukua udhibiti wa hospitali za umma.
Wafanyakazi wengine wa viwanda vya kutengeneza na kukarabati magari walianza mgomo jumatano wakidai nyongeza ya asilimia 15 ya mshahara..