“Tunafuatilia kwa karibu na tunasikitishwa sana na ghasia zinazoendelea huko Sudan Kusini na Congo, Trump alisema katika mkutano wa chakula cha mchana siku ya Jumatano akiwa na viongozi wa Afrika pembeni ya mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa. Mamilioni ya watu wako katika hatari na tunaendelea kutoa msaada wa kibinadamu lakini matokeo ya kweli ya kusitisha janga hili yatahitaji utaratibu wa amani unaoongozwa na viongozi wa kiafrika na ni nia ya dhati ya kweli ya pande zote zinazohusika”.
Rais Trump alisema balozi Haley atajadili hali ya mgogoro na suluhisho na lililo muhimu sana ni kuzuia, alisema Trump. Sudan Kusini imegubikwa kwa mwaka wa nne na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimewakosesha makazi watu wapatao milioni nne wakati Congo inashuhudia ongezeko la ghasia kutokana na mapambano ya kijamii na sintofahamu juu ya lini nchi hiyo itafanya uchaguzi. Rais wa Congo, Joseph Kabila ameendelea kuwepo madarakani licha ya muda wake kumalizika tangu Disemba mwaka 2016.
Rais Trump pia alieleza kuwa mataifa sita kati ya 10 duniani yenye uchumi unaokuwa haraka sana yapo Afrika. Afrika ina nafasi nzuri ya biashara, nina marafiki wengi sana wanakwenda nchini humo wakijaribu kupata utajiri, alisema Trump.