Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 16:41

Mgogoro mpya wazuka baina ya IEBC, Nasa


Raila Odinga na mgombea mwenza wakipokelewa na IEBC katika mchakato wa uchaguzi wa Agosti 2017
Raila Odinga na mgombea mwenza wakipokelewa na IEBC katika mchakato wa uchaguzi wa Agosti 2017

Wakati matayarisho ya uchaguzi wa urais Kenya yanaendelea, mgogoro mpya kati ya Muungano wa Upinzani wa Nasa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) umeibuka.

Mgombea urais wa muungano wa National Super Alliance, NASA, ametofautiana na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka, IEBC, iwapo kulikuwa na makubaliano yoyote baada ya mkutano kati yao uliofanyika katika ukumbi wa Bomas of Kenya siku ya Jumanne.

Raila Odinga amesema kuwa hakukuwa na maafikiano yoyote na ni kwa sababu hiyo ambapo wafuasi wa muungano huo wataendelea na maandamano ya kuishinikiza tume hiyo kufanya mabadiliko kadhaa kabla ya uchaguzi wa urais wa tarehe 26 mwezi huu.

Hata hivyo, mwenyekiti wa tume hiyo, Wafula Chebukati, aliwaambia wanahabari kwamba mkutano huo ulileta tija.

Wakati huo huo, Wakenya kutoka makundi mbalimbali kwa siku ya pili mfululizo wanaendelea kufika mbele ya kamati maalum ya pamoja ya bunge la Kenya kuwasilisha maoni yao kuhusu mswada unaoazimia kufanya marekebisho katika vifungu kadhaa kuhusu sheria za uchaguzi.

Kwa upande wao wabunge wa upinzani wameonekana kukataa katakata kujihusisha na shughuli za kamati hiyo.

Lakini hilo halikuwakatisha tamaa wabunge wa Jubilee kuendelea kuyasikiliza maoni ya makundi mbalimbali ya wakenya.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti Jumatano ni zamu ya makundi ya vijana, wanawake, mashirika ya kijamii, kibiashara na baadhi ya wanasiasa waliobwagwa katika uchaguzi mkuu.

Hata hivyo kipengele ambacho kinataka naibu mwenyekiti wa tume ya uchaguzi au kamishna yeyote atakayechaguliwa na makamishna wa tume hiyo apewe uwezo wa kuchukua nafasi ya uenyekiti wa IEBC iwapo kwa sababu yoyote ataondolewa, kimepokelewa kwa hisia tofauti katika mswada huo.

Kwa mfano Alex Otunga anasisitiza kuwa huenda pana mchezo ambao unaendelea.

Aidha, wawakilishi wa wanawake kutoka makundi kadhaa walifika mbele ya kamati hii kutoa mapendekezo yao wakisisitiza kuwa ni sharti pawepo na sheria itakayowakaba koo wanaohujumu mchakato mzima wa uchaguzi.

Miswada hii iliyowasilishwa na wabunge wa chama tawala cha Rais Uhuru Kenyatta, iwapo itapitishwa katika viwango vyote na kuwa sheria, katika kura ya Urais ijayo, tume ya uchaguzi itatakiwa kutangaza matokeo ya kura hiyo sambamba kupitia mfumo wa kielektroniki na mfumo usio wa kielektroniki kutoka vituo vyote vya upigaji kura.

Na iwapo mifumo hiyo miwili itatofautiana, mfumo usiokuwa wa kielektroniki ndio utakaoidhinishwa. Vile vile, matokeo ya kura hiyo hayatabatilishwa iwapo mfumo wa kielektroniki haukutumika kutangaza mshindi.

Hata hivyo upinzani, wakilishi wa makanisa pamoja na mabalozi wa nchi za kigeni wameonekana kujitenga na mswada huo.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya.

XS
SM
MD
LG