Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 06, 2024 Local time: 12:04

Malawi haitoandaa mkutano wa AU


Rais wa Malawi Joyce Banda akizungumza na waandishi wa habari katika mji mkuu Lilongwe, Malawi
Rais wa Malawi Joyce Banda akizungumza na waandishi wa habari katika mji mkuu Lilongwe, Malawi

Malawi ilikosolewa na makundi ya kutetea haki na wafadhili wa kimataifa walipomkaribisha bwana Bashir kwenye mkutano wa kikanda mwaka jana wakati wa utawala wa marehemu Bingu Wa Mutharika.

Makamu Rais wa Malawi ametangaza kwamba Umoja wa Afrika-AU utalazimika kubadili mahala pa kufanyia mkutano ujao wa viongozi wa Afrika kufuatia uamuzi wa Malawi kukataa kuwa mwenyeji na kumpokea Rais Omar Al Bashir wa Sudan kwenye mkutano huo.

Rais wa Malawi Joyce Banda alisema watalazimika kumkamata Rais Bashir kutokana na hati ya kukamatwa kwake iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu-ICC ikiwa ataitembelea nchi hiyo.

Akizungumza kwenye redio ya taifa Makamu Rais wa Malawi, Khumbo Kachali alisema baraza la mawaziri lilikutana Ijumaa na kuamua hawatokuwa wenyeji wa mkutano wa viongozi wa afrika uliopangwa kufanyika mwezi ujao nchini humo.

Alisema mawaziri walichukua uwamuzi wao kutokana na alichokisema ni “kwa ajili ya maslahi bora ya wamalawi”.

Hapo mwanzoni Malawi iliiomba Umoja wa Afrika kutomualika Rais Omar al-Bashir wa Sudan lakini AU ilieleza kwamba si juu ya nchi mwenyeji wa mkutano kufanya uamuzi kama huo. Kachali alisema Umoja wa Afrika ulimueleza kwamba mkutano huo utahamishwa na kufanyikia Addis Ababa nchini Ethiopia.

Billy Banda mkuu wa kundi la haki za binadam la Malawi Watch anasema uamuzi wa kufuta mkutano unaleta faida na hasara kwa Malawi.“Malawi kama nchi imechukua uamuzi kwa sababu inataka kuonesha uwajibikaji wa pamoja kwa kushirikiana na jumuiya ya kimataifa juu ya suala la Bashir. Lakini kwa wa-Malawi tunawasi wasi kwa sababu wamalawi wengi wangepata nafasi ya kubadilishana mawazo na kuzungumza na viongozi wengine katika sekta za makundi yasio ya kiserikali, katika sekta ya biashara”.

Malawi ina sababu za kuwa na wasi wasi kuhusu athari zitakazotokana na ziara ya bwana Bashir. Nchi hiyo ilikosolewa na makundi ya kutetea haki na wafadhili wa kimataifa walipomkaribisha bwana Bashir kwenye mkutano mwingine wa kikanda mwaka jana wakati wa utawala wa marehemu Bingu Wa Mutharika.

Idara ya maendeleo ya kimataifa ya Marekani ilichukua uamuzi wa kusitisha msaada wa dola milioni 350 kwa Malawi kutokana na ziara hiyo.

Bw Mutharika alifariki kutokana na mshtuko wa moyo na aliyechukua nafasi yake bibi Joyce Banda amekua akijaribu kuimarisha uhusiano na jumuiya ya kimataifa.

Kiongozi wa upinzani nchini Malawi Kamuzu Chibambo wa chama cha People’s Transformation anasema anaunga mkono uamuzi wa serikali na kuilaumu AU kwa kutokuwa tayari kufikia maridhiano.

XS
SM
MD
LG