Kampeni za mwisho mwisho zinafanyika kote nchini Kenya kabla wananchi hawajapiga kura ya maoni kuhusu katiba mpya nchini humo Jumatano.
Utafiti wa maoni ya watu unaonyesha Wakenya wengi wanaunga mkono rasimu ya katiba ambayo pia inaungwa mkono na Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga.
Katiba mpya itapunguza madaraka ya rais, na kutoa madaraka zaidi kwa serikali za mitaa na kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri hadi mawaziri 22 tu. Miongoni mwa mabadiliko mengine katiba mpya itaunda baraza jipya katika bunge na kuondoa nafasi ya waziri mkuu.